Bibi Namkunda Nampombe Kashimbiri's Life Sketch -- Kiswahili
NAMKUNDA NAMPOMBE KASHIMBIRI (NEE KAJIRU)
(1916 – 2014)
Utangulizi
Uchambuzi wa kipindi cha muda unaokaribia sana karne ndio masimulizi ya maisha ya Namkunda Nampombe Kashimbiri (NNK). Baba yake alikuwa Kajiru mwana wa Mrekwa aliyeweka makazi yake Vugwama, kijiji kilichopo nyuma ya milima mashariki mwa Suji. Mama alikuwa Nankoo Semwaya kutoka kijiji cha Kitunda. Mama huyu alizaliwa mwaka 1916 katika kijiji cha Nkogo, tarafa ya Suji Wilaya ya Same Upareni, Tanzania. Same na Mwanga ndizo wilaya mbili za Upare katika mkoa wa Kilimanjaro. Kuzaliwa kwa Namkunda kulitokea wakati wa zama za ukoloni wa Kijerumani; karibia miaka miwili baada ya kuanza kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Alipozaliwa, kuzaliwa kwa mtoto wa kaka yake, Ruth pia kulitangazwa. Baba yake Ruth ni Isae Stefano Kajiru ambae ni kaka yake NNK kwa upande wa baba. Kajiru alikuwa mtu wa wake wengi akiwa na wake watano ambao majina yao ni Mshinwa, Shode, Shiragi (kutokana na mila ya kurithi wajane baada ya Chambi kufariki), Nashinwa na mwisho Nankoo na alibarikiwa kupata jumla ya watoto 42.
Katika muda usiofahamika, Kajiru na kaka yake Chambi, walimwacha baba yao na kuhama kutoka Vugwama. Baada ya hapo Kajiru alijiimarisha kama mzee wa familia yake huko Nkogo na Chambi akawa mzee wa familia yake katika kijiji cha jirani cha Chairika. Kajiru alifahamika kuwa na sauti nzito na yenye nguvu. Alikuwa ni mmojawapo kati ya washauri wa chifu. Ilisemekana kuwa kikao hakikuanza mpaka Kajiru ( aliyeitwa jina la utani la Ngoma Kwaya) awe amekaa kitini mwake. Ndugu hawa wawili walihama kijiji chao cha kuzaliwa wakiambatana na watu wengine wa familia zao kutokana na kuwepo kwa magonjwa mengi huko. Katika siku hizo watu waliamini kuwa mkondo wa hewa ya joto uliotokea kwenye uwanda wa juu wa milima ya mashariki mwa Vugwama, yaani Bendera, Kihurio na Ndungu ndio uliochangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa magonjwa hayo. Vugwama ilikuwa kwenye ukanda wa juu na ilikuwa na hali ya ubaridi wakati wote wa mwaka.
Mama yake NNK (Nankoo), akiwa ndiye mdogo katika familia kubwa yenye wake wengi, alilazimika kudhihirisha uwezo wake. Nankoo alibarikiwa kupata watoto tisa na kati ya hao ni ndugu saba walioishi. Ndugu hao saba ni Namnyai, Nakizwa, Chali, Nanzano, Nampombe, Kashera na Kangula na kati yao Chali na Kashera walikuwa wa kiume. Kupata watoto, na hakika kuwa nao wengi, ilikuwa ni muhimu sana kwa kutambulika na kukubalika kwa mwanamke aliyeolewa katika ukoo. Kwa umuhimu huo huo, Nankoo alikuwa mchapa kazi sana kulisha watoto wake na mumewe. Kila mwanamke aliyeolewa alitegemewa kulisha watoto wake vizuri na kuwapatia mahitaji yao mengine ya msingi. Wanaume walitegemewa kuandaa nyumba (nyumba ya tope iliyoezekwa kwa nyasi) kwa ajili ya kila mke aliyekuwa naye, mashamba ya kilimo, kuwajibika kwa kulisha na kujali wanyama wa kufugwa na kwa ujumla kupewa uongozi na madaraka.
Kizazi cha leo kinaweza kushindwa kuelewa kikamilifu mwenendo wa familia kubwa kama hiyo ya mfumo wa kurithi kutoka upande wa baba na ya wake wengi ambapo mpendwa wetu alizaliwa na kulelewa katika utoto wake wa awali. Nankoo alikuwa msimamizi mkubwa wa nidhamu kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na watoto wake, wengine wao pia walikiri kufanana au angalau kukaribia mama yao. Bila shaka, Namkunda, mama mpendwa huelezea kwa kumbukumbu za kupendeza jinsi ambavyo familia yao kubwa iliishi pamoja kwa upatanifu, heshima na upendo katika mfumo wa ukoo wao. Hata hivyo kwa masikitiko, anazidi kusema “kwa nini ni mimi peke yangu niliyebakia katika kizazi changu”, akiwa na umri wa miaka 97 ni yeye peke yake aliye hai kati ya watoto 42.
Uzoefu wa Utoto
Kama mtoto, Namkunda alifaidi uhuru mwingi. Hakuweza kuelezea kikamilifu kwa nini ilikuwa hivyo. Hata hivyo, anaamini kuwa mmoja wa watoto wadogo kulichangia, ilikuwa ni desturi kwa kaka na dada wakubwa kufanya kazi za nyumbani zaidi pamoja na mama yake. Baba yake alikuwa mganga maarufu katika jamii. Aliheshimiwa sana na alikuwa na wateja wengi waliomfikia mara zote wakitafuta huduma zake. Watoto wadogo walikuwa maeneo ya nyumbani wakati mwingi wakiitika wito wake kadri alivyokuwa akihudumia wateja wake. Inaonekana kuwa mama mpendwa huyu alikuwa katika vitabu vyema vya baba yake kiasi cha kuaminika na kupewa kazi ndogo ndogo karibu na baba yake. Matukio muhimu yafuatayo yataonyesha jinsi ambavyo baba yake alionyesha upendeleo mkubwa kwake, angalau kama alivyoona yeye.
Tukio la kwanza lilikuwa wakati mama yetu Namkunda Nampombe Kajiru alipokuwa amekataa kutobolewa masikio yake. Inashangaza kuwa baba yake alimwachia iwe kama alivyoamua. Tukio la pili lilikuwa wakati alipokuwa anakaribia muda wake wa kanuni na matambiko ya kufundwa (kugerwa ngasu). Kipengele kimojawapo muhimu cha utaratibu huu mahsusi kilihusu ukeketaji. Katika tukio hilo, alikataa kupitia kaida hiyo. Baba yake kwa mara nyingine alikubaliana na mapenzi yake. Kama baba yake, Kajiru alikuwa na haki na uwezo wa kulazimisha binti yake akubali, lakini hakufanya hivyo. Kwa maoni yake, alihusisha ujasiri wa baba yake kwa sehemu na maarifa yake ya tiba na uwelewa kuwa jadi kama hizo hazina maana yoyote au manufaa kwa afya yake atakapokuwa mwanamke mzima. Zaidi ya hilo, alisititiza kuwa vitendo vyake na maamuzi katika maisha yake na kazi, yalitokana na tabia zake za kurithi na kusadiki kwake imani na elimu ya Kikristo. Kwa hiyo, kisa hiki kifupi kinatarajiwa kuonyesha matokeo ya uzoefu huu kwake kama mtu, mwanamke, mke, mama, mwalimu na raia mwaminifu kwa ujumla.
Maisha ya Shule na Ukristo
Mama yetu mpendwa Namkunda alikuwa na bahati ya kuwa na kaka na dada waliohudhuria shule zilizoanzishwa na wamishonari wa Kijerumani. Kaka yake (mama tofauti) Stefano Kajiru alikuwa mwalimu katika Shule ya Kijiji cha Gonjanza, kilichopo karibia kilomita mbili kutoka kijiji cha Nkogo na baadaye alikuwa Mhudumu wa Kanisa. Alikuwa amedhamiria kufanya kama dada yake mmoja aliyekuwa ameanza shule, amesadiki Ukristo na amehamia kwenye kituo cha umishonari cha Suji. Mama yake alipinga hatua hii ya binti yake mwingine kusadiki Ukristo au hata kwenda shule. Pamoja na tofauti hizi katika familia, aliandikishwa katika daraja la 1 katika Shule ya Misheni ya Gonjanza katika umri mdogo. Baada ya hapo alifanikiwa kupata uhamisho kutoka Shule ya Misheni ya Gonjanza kwenda Shule ya Misheni ya Suji na mwaka uliofuatia kutimiza azma yake ya kuukubali Ukristo.
Mama yake hakufurahishwa na alimchapa sana na zaidi ya hapo alimkataza kuwa Mkristo (hasa kabla hajafundwa). Kwa hakika, ilifikia wakati wa kusukumwa mara kadhaa na kusababisa NNK kuacha kuufuatilia Ukristo kwa muda. Hata hivyo mwishowe, NNK alitoroka na akaenda Suji. Baada ya hapo alipokelewa katika shule na kupangiwa kuishi katika bweni la wasichana. Nyakati fulani mama yake alitembelea Shule ya Suji ili kumtoa shuleni na pia kumwadhibu. Mwisho wake, NNK alipata ushindi akifuatilia imani yake mpya na elimu kwa wakati mmoja. Alibatizwa mwaka 1932 katika Kanisa la Waadventista Wa Sabato Suji Misheni.
NNK alipenda shule na alifanya vizuri sana katika kazi zake za shule. Nafasi yake katika darasa daima ilikuwa wa kwanza, pili au tatu kati ya wanafunzi thelathini hadi arobaini. Kati ya aliosoma nao darasa moja alikuwa Lea Mnyuku ambaye baba yake alikuja kuwa Chifu wa Suji kufuatia kuanzishwa kwa utawala wa machifu na utawala wa Waingereza uliojulikana kama “the Indirect Rule”, yaani utawala wa kuwatumia viongozi wananchi usio wa moja kwa moja, Wasichana wachache walihudhuria shule na wale waliomaliza shule walijiunga na mafunzo ya ualimu na kuhitimu kama walimu katika fani iliyokuwa ya wanaume kwa wakati huo. Chuo cha Ualimu cha Suji kilikuwa kikitoa walimu waliokuwa wakipata vyeti vya Serikali kuanzia 1927. Hata hivyo, Damari Kangalu alikuwa mwalimu wa kwanza mwanamke aliyefuzu kutoka katika Chuo cha Ualimu cha Suji mwaka 1931, pia akiwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanganyika kupata hadhi hiyo. Awamu ya pili ya walimu wenye sifa wanawake walihitimu mwaka 1933. Hao walikuwa Namkunda Nampombe Kajiru na Lea Mnyuku (binti wa Chifu wa Suji kwa wakati huo). Hii ina maana kuwa wahitimu wengine wote kutoka mwaka 1927 hadi 1933 walikuwa wanaume.
Ndoa na Matokeo Yake
Baada ya kufuzu kama mwalimu, NNK alichumbiwa na kijana aliyeitwa Rafaeli Kashimbiri ambae pia alikuwa amefuzu kama mwalimu kutoka shule hiyo hiyo. Kwa hiyo wawili hawa waliunganishwa katika ndoa takatifu mwaka 1934 huko Suji Misheni. Ilikuwa ni harusi maarufu kwani katika historia yote ya kanisa, ilikuwa haijatokea wanandoa wengi wakristo kufungiwa ndoa kwa wakati mmoja. Katika tukio hili, wanandoa watano wakristo walifunga ndoa kwa wakati na mahali pamoja. Wanandoa hawa walikuwa ni Eliamani Kachua na Maria Nankware Kilonzo, Rafaeli na Namkunda Kashimbiri, Stefano Selanyika na Neemaeli Singo, Dani Sapo na mkewe na Elisante Mcharo na mke wake. Wanandoa wote wa ndoa hizo tano walisadiki Ukristo na kupata elimu kutoka katika shule za kanisa na baadae walikuwa waajiriwa wa Kanisa na au wamishonari. Hiki ndicho kitu kimoja kinachosababisha maumivu mengi kwa NNK leo anapokumbuka wenzake ambao wamefariki. Kila wakati anapokutana na wale wa uzao wa wanandoa hao, machozi hulenga lenga katika macho yake.
Lilikuwa ni jambo la kawaida kwa wanawake wafanyakazi kuacha kazi zao mara tu walipoolewa. Hiyo ilikuwa ni katika miaka ya 1920 na 1930. Hii inaweza kufanyiwa utafiti katika historia jinsi taratibu zilivyokuwa kuanzia wakati huo katika jamii yote. Wakati NNK alipoolewa, mwenzi wake wa ndoa, Rafaeli alikuwa tayari akifundisa huko Kihurio. Hali ikiwa hivyo, alilazimika kwenda Kihurio ili akae pamoja na mumewe. Inasikitisha kusema, hakupewa nafasi yoyote ya kazi kama mwalimu kwasababu ilichukuliwa kuwa mwanamke anapoolewa jukumu lake lilikuwa ni kubakia na kufanya kazi nyumbani. Kihurio iko katika tambarare za Eneo la Mkomazi Upare. Hali ya hewa ya sehemu hiyo ilikuwa tofauti kabisa na ile ya Suji. Ilikuwa joto na uwepo wa mbu ulikuwa mkubwa, na ndivyo ilivyo hadi siku ya leo. Hii ikiwa hivyo, NNK aliambukizwa malaria mara kwa mara ikiathiri afya yake na uwezo wa kupata ujauzito wa mtoto. Kufuatia matukio haya katika afya ya mke wa Rafaeli, waajiri wake waliamua kuhamishia Mamba nafasi yake ya kazi, juu milimani. Kati ya 1936 na 1941, Rafael, mumewe, alifanya kazi Mamba na baadae Vugwama (sehemu aliyozaliwa baba yake NNK Kajiru) lakini mkewe alibakia nyumbani. Kwa wakati huu katika historia, familia hii changa ilibarikiwa kuwa na watoto watatu ambao kwa majina ni Mary, Ferdinand na Nankoo.
Mishahara ya walimu Tanzania ilikuwa chini sana na haikuendana na majukumu ya kazi yaliyokuwa juu wakati mishahara ikiwa chini. Akina Kashimbiri kama walimu wengine walivyofanya ilibidi kutegemea ardhi wakilima mazao kwa ajili ya chakula, wakifuga kuku, mbuzi, kondoo na ng’ombe kujiongezea kipato zaidi ya mishahara na pia wakifundisha. Ilikuwa kawaida kuwa na wafanyakazi wa nyumbani, kama walezi wa watoto, kuwalea watoto na kufanya kazi nyingi za ndani. Hawa wasaidizi waliweza kuwa ndugu wa karibu au vinginevyo, na mara zote walichukuliwa si kama watumishi wa ndani lakini kama sehemu ya familia. Matokeo yake, wengine wao walijifunza utamaduni na mfumo wa maisha mpya wakifundishwa na wenyeji wao. Mara nyingi, wao na watoto wao walisadiki ukristo. Hakika, mwalimu huyu mashuhuri wa kike aliweza kukumbuka watu wa jamaa zake karibia kutoka kila kituo walipoishi yeye na mumewe. Jamii iliyozunguka shule ambapo waliishi ilikuwa na watoto ambao waliotamani kupata elimu. Kama desturi, Nyumba ya NNK haikupungukiwa watoto waliokaa kwa muda mrefu na familia yao ili kupata msaada kwa ajili ya elimu kwa kuwa wazazi wao walishindwa kuwasaidia. Hata hivyo, yeye na mumewe kamwe awakuajiri mtumishi wa ndani katika maisha yao. Watoto wote waliokaa nao walifanya hivyo ili kupata fursa ya kusoma.
Kufundisha Ilipohitajika
Mamlaka ya Kanisa katika Upare haikuona mbali kutokana na kuwa walipoteza faida ya kutumia mwalimu mwenye sifa kwa sababu tu kuwa alikuwa ameolewa. Hii ilikuwa zaidi hivyo, kituo cha kazi cha wanandoa hao kilipokuwa Mamba. Elimu ya Kikristo katika milima ya Upare na pengineko nchini ilikuwa katika uchanga wake. Elimu kwa wasichana ilikuwa si tu kitu kipya bali pia kitu kilichokumbwa na upinzani kutoka kwa jamii. Kwa desturi, juu ya matarajio yote, wanawake walikuwa ni wa kuolewa na kulea familia. Pamoja na hayo, ukiristo ulifungua milango kwa ajili ya elimu ya wasichana kama ilivyokuwa kwa wavulana. Shule huko Suji, Kihurio, Mamba and Vugwama zilikuwa za mseto. Changamoto hii ilifanya uongozi kufikiria kwa uzito juu umuhimu wa kuwa na walimu wa kike katika kila shule. Zaidi ya hapo, walimu wa kike walikuwa wachache sana katika kipindi hiki. Kwa hakika, mwalimu kama NNK angepaswa kupelekwa shule tofauti kila wakati ambapo kungetokea hitaji la walimu wa kike.
Zaidi ya hapo, shule ya bweni ilikuwa tayari iko Ikizu, shule iliyokuwa upande wa kusini mashariki mwa Ziwa Victoria ambapo matroni mwangalizi alikuwa Ngwanangenji. Kwa kuwa Ngwanangenji hakuwa mwalimu mwenye sifa, wakaguzi wa Serikali walikuwa wameagiza kwamba sehemu ya shule ya bweni kwa upande wa wasichana ifungwe mpaka hapo mwalimu wa kike mwenye sifa atakapoteuliwa kushika nafasi hiyo. Kutokana na agizo hilo, mwaka 1942 NNK aliombwa kwenda Ikizu kama Matroni wa shule ya bweni ya wasichana na pia kutumika kama mmoja wa walimu wake. Kwa kushukuru zaidi, alikuwa aambatane na mume wake. Kando ya kuwa matroni, alipewa majukumu ya kufundisha kama walimu wenzake wa kiume. Hivyo alifanya kazi nje ya maeneo aliyoyazoea ambapo desturi na mila zilikuwa ngeni sana kwake na mumewe pia.
Nafasi hiyo ya kazi ilikuwa changamoto katika maisha yake ya awali kikazi. Bila kuonekana kuhukumu, anasititiza kuwa makabila ambayo wanafunzi wao walitoka kama vile Waikizu, Wazanaki, Waikoma, Wajita, Wakurya and Waluo kuorodhesha machache, hawakuwa na heshima kwa wasichana na wanawake nje ya nyumbani. Zaidi ya hapo alisema, “Wanawake walinyanyaswa, walitendewa vibaya na kwa ujumla hawakuheshimiwa kati ya watu wa asili wa sehemu ile”. Hii ikiwa ndo hali, elimu kwa wanawake haikuwa na maana ya kutosha au kufikiriwa yenye manufaa na jamii. Hii ilimaanisha kuwa hakukuwa na msukumo mkubwa kwa wazazi wengi kupeleka watoto wao wa kike shuleni. Kwa nyongeza, hata wavulana waliokuwa wanakwenda shule kwa ujumla walitegemewa kuwa wafugaji wazuri. Kutokana na mazingira haya, NNK anasema, mtu hawezi kushindwa kuona alivyokuwa anatazamwa na jumuiya ya wanaume wa Ikizu. Alikuwa kama muasi katika jamii na kwa kujisikia na kuamini kwao ilikuwa ni kuwa asifundishe au kushikilia kazi inayohusu uangalizi kama hiyo kwa watoto wao wa kike shuleni.
NNK alitumia saa nyingi akielezea juu ya hali hii, ambayo leo inaweza isitambulike kikamilifu. Jamii iliwadharau wanawake na walimu wa kiume waliwadharau walimu wa kike na inasikitisha kusema, hata kanisa liliungana nao. Vibaya zaidi, sera ya malipo ya Kanisa ilikuwa kwamba wanawake walikuwa wapokee 80% ya malipo ya wenzao wa kiume kama mshahara. Haikujalisha hata kama wenzao wa kiume wangefanya kazi sawa na wakiwa na sifa sawa. Hii ilichangia katika kutoridhika na hasira na wakati mwingine hilo lilikuwa haliwezi kuepukwa.
Kama matroni Ikizu, matroni alikuwa na upendeleo wa kupata chakula pamoja na wanafunzi bure bila malipo. Mmoja angefikiria kuwa utaratibu huu unatoa mafao ya ziada kwa wale waliokuwa wanatekeleza majukumu ya ziada kama umatroni. Lakini kwa kuwa matroni huyu alikuwa ameolewa na ana watoto, ilikuwa haiwezekani kwake yeye kula na wanafunzi wakati wote. Hivyo iliamuliwa kuwa atapata mgao wa chakula ambacho hakijapikwa, sawa na kiasi ambacho wanafunzi wangepata kila mwezi kupeleka nyumbani kwake. Kwa uchache mwalimu mmoja wa kiume mlalamishi na mwenye wivu alitoa malalamishi yake kwa uongozi juu ya suala hili. Matokeo yake utaratibu huo ulifutwa na ingawa alikuwa ni matroni, ilibidi asiendelee kupata mafao hayo. Uonevu ndilo neno. Hata hivyo, maadili yake ya Kikristo yaliyoko akilini mwake yanaonekana katika maoni yake kuhusu hili, “bado tuko katika dunia hii ya dhambi. Bado hatupo mbinguni; kwa hiyo vitu vibaya bado vipo kwa wingi hata leo”.
Utume ulikuwa unapanuka kwenye kanda hii. Shule mpya ya wasichana ya bweni ilikuwa karibu kufunguliwa. Ilikuwa wazi tena kuwa mwalimu wa kike alikuwa anahitajika kabla ya ruhusa kutolewa na Serikali ya kufungua shule hiyo mpya, vinginevyo shule hiyo mpya isingeweza kuandikisha wasichana. Mama huyu mwalimu alikuwa anahitajika sana tena. Ndiye aliyekuwa mwalimu wa kike mwenye uzoefu kuliko wote aliyekuwepo ambaye angeweza kuhamishiwa Utimbaru kwa muda. Ilibidi apelekwe huko kufundisha wasichana kabla ya shule kuanza. Angerudi tena Ikizu baada ya mwingine wa kuchukua nafasi yake kupatikana.
Wakati wa miaka ya awali ya elimu ya shule katika nchi hii, umri maalum uliotamkwa haukuwa kigezo cha kuanza shule. Shule za Ikizu, Utimbaru na hata za Upare zilikuwa na utaratibu uliofanana wa kuingiza wanafunzi. Zote zilikuwa na wanafunzi waliokuwa watu wazima kuanzia madarasa ya daraja I. Wanafunzi wengine wa kiume walikuwa wameoa na wana watoto kabla ya kuanza shule. Hii ilitia wasiwasi kwa mwalimu wa kike. Katika mazungumzo alisema moja kwa moja kuwa ilimbidi mwalimu mwanamke kuwa mwenye kutumia mbinu za ziada, mwerevu, wa busara na mwenye kuheshimu lakini mwenye msimamo katika kutunza sheria za shule. Ilimwia vigumu sana kuendeleza nidhamu wakati wote kwa kuwa wavulana walikuwa ni matokeo ya jamii, hata hivyo isiyoheshimu wanawake.
Anakumbuka tukio ambapo siku moja mwafunzi mmoja wa kiume mrefu na mwenye maumbile makubwa alikuwa amesimama mbele yake aliyekuwa jeuri na asiye na heshima. Anaelezea zaidi alivyojisikia kutishwa na akakasirika sana na hivyo ilibidi kuchukua hatua. Aidha alikuwa aonyeshe madaraka au anywee, uchaguzi ambao ungegusa mwonekano wake mbele ya wanafunzi wengine. Alisubiri kwa muda mfupi sana ambapo mwanafunzi huyu wa kiume alikuwa ameangalia kwingine, akamrukia na kutupa mikono yake shingoni mwake na kwa nguvu zake zote akamsukumiza chini ardhini. Mhusika alikuwa katika mshutuko na wanafunzi walioshuhudia walishangaa katika mshutuko kama alivyokuwa yeye. Anasema tendo hilo halikuwa la kujirudia, lilikuwa ni tendo lililotokea bila kutarajia na hakulirudia tena. Hata hivyo, hii ilimletea heshima muda wote aliofundisha Ikizu.
Katika muda wake wote wa kazi ya kufundisha, alijitahidi kufanya vizuri katika chumba cha darasa kadri alivyoweza kwa kutayarisha masomo yake vema kwa wakati na muhtasari wa somo ukiwa tayari wakati wote. Utaratibu huu haukumpa tu amani akilini mwake lakini pia ulifurahisha wanafunzi wake ambapo wengine wao walifanikiwa sana maishani. Kati ya wanafunzi wake walikuwa ni Thomas Lisso ambaye baadae alikuwa Mkuu wa Shule, Mhudumu Kanisani na halafu Mbunge; na Raphael Megera aliyejiunga na shule baada ya kutumika katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia akiwa mtu mzima, ingawa baadae alipata mafunzo kama Mhudumu Kanisani, Mhasibu mwenye uwezo na vile vile Mkaguzi. Wakati akifanya kazi Ikizu, alipata watoto wengine wanne ambao majina yao ni: Aggrey, Pheno, Washington and Peter.
Imani Mbele ya Umaarufu
Katika miaka ya mwanzo ya 1950, Mwalimu Julius K Nyerere, akiwa kiongozi wa Tanganyika African National Union (TANU), binafsi alimwendea mwalimu huyu mpendwa mwanamke na alimshawishi kujiunga na Chama kama kada wa kudumu. Nyerere alielezea mapambano ya uhuru kwa watu wote wa Tanganyika. Alimgusia pia kuwa TANU ilikuwa na makada wachache wa kike kwa ajili ya uongozi- sharti ambalo lilikuwa muhimu kwa ajili ya mafanikio yake ya baadae. Pamoja na sababu hizi za kushawishi na fursa, NNK alikataa ombi hilo. “Lilikuwa ni Kanisa lililonipa elimu na kazi”, alielezea kwa msititizo. Kwa hiyo alijisikia kuwajibika kuendelea na huduma yake kwa Kanisa.
Safari kwenda Mbeya
Vituo vya Umishenari na shule zilipatikana Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, Mkoa wa Ziwa, Mikoa ya Magharibi na Nyanda za Juu Kusini za nchi. Akiwa ametumikia kwa miaka 14 katika eneo la Ziwa Victoria, mwalimu mwanamke mpendwa alihamishiwa Mbeya mwaka 1956. Hata hivyo, itambulike kwamba Kanisa halikuwa na shule za wasichana za bweni Mbeya. Hata hivyo, kulikuwa na wasichana walioandikishwa katika shule na fursa ya kuboresha elimu ya wasichana katika eneo hilo ilikuwa ya kutia moyo. Kwa hakika, wakazi wa Mbeya walikuwa na bahati kuwa na mwalimu mwanamke mwenye uzoefu kama huyu. Hii itaamsha zaidi haja ya majengo na vifaa vya shule za bweni za wasichana katika eneo hili. Kama ilivyokuwa katika Kanda ya Ziwa, Mbeya ilikuwa na tofauti nyingi za kitamaduni ambazo mwanamke huyu mwalimu ilibidi ajifunze na kuzikubali. Kufikia wakati huu, kazi yake ya kufundisha ilikuwa imemfanya mmoja kati ya walimu wa kike waliosafiri sana ndani ya nchi. Hizi zilikuwa siku ambazo usafiri wa barabara na reli ulikuwa haujaendelea kikamilifu. Huduma za Posta, mawasiliano ya simu au vinginevyo yalikuwa haba sana nchini. Kwa hiyo akina Kashimbiri walikuwa wametengwa kutoka kwa jamaa za walikotoka kwa vipindi virefu vya muda kila mwaka.
Katika Njia Panda
Ni bahati mbaya kwamba kazi ya akina Kashimbiri huko Mbeya ilifikia mwisho mbaya baada ya miaka mitatu ya kuwepo huko. Bwana Rafaeli Kashimbiri alikuwa ameshitakiwa kwa utovu wa nidhamu na hatua za kinidhamu zilichukuliwa na kusababisa kukosa kazi yake ya kufundisha katika shule zilizokuwa zinaendeshwa na Kanisa. Siyo tu kwamba aliachishwa kazi bali alipewa amri ya kuondoka katika maeneo ya shule na kuzuiliwa kuingia tena. Hali ikiwa hivyo, mke wake na watoto wake ilibidi wabakie katika mji wao, uliokuwa katika maeneo ya shule. Tendo hili lisilokuwa na mantiki lilionekana kutovumilika kwa familia kufikia kwamba Bwana Kashimbiri alirudi nyumbani chini ya kinga ya giza mara kadhaa.
Gumzo lilisambaa juu ya uvunjifu wa amri na mmishonari aliyekuwa mkuu katika Kituo cha Umishonari cha Mbeya alitafuta ufafanuzi kutoka kwa mke wa Rafaeli Kashimbiri. Aliweka bayana kuwa mumewe alikuja nyumbani kuona familia yake. Matokeo yake naye alifukuzwa kutoka katika kazi yake ya kufundisha. Mume na mke wote walikuwa hawana kazi; walikuwa na watoto wa kulea; walikuwa hawana makazi na walikuwa zaidi ya kilomita 1000 kutoka mahali walipozaliwa Upareni. Kulikuwa hakuna uchaguzi ila mke alilazimika kusafiri kurudi nyumbani peke yake na watoto mwaka 1959. Usafiri wake kurudi nyumbani uligharimiwa na uongozi wa misheni. Wakati huo, mtoto wao wa mwisho Margaret alikuwepo kwenye familia. Siku aliyotenganishwa na mumewe ilikuwa mwanzo wa ndoa ya uhamishoni mpaka mumewe alipozikwa Mbeya mwaka 2000.
Enzi Mpya
Akiwa ametenganishwa na mumewe na baadhi ya watoto wake wakubwa, NNK alikabiliwa na maisha ya usoni ya kuogofya na shida. Akiwa amekata tamaa, alikutana na mkuu wa misheni ya Suji kuona kama angeweza kupata kazi yoyote ya kipato kulisha watoto wake. Hadi wakati huu, ilikuwa haieleweki kwanini afukuzwe kutoka kazini bila shitaka. Mwisho wake, haki ilishinda na alirudishwa katika kazi yake ya kufundisha. Alipelekwa katika Shule ya Msingi ya Kwamshitu, siyo mbali sana kutoka Vugwama ambapo aliwahi kufanya kazi katika miaka yake ya awali kikazi. Vugwama ingekuwa si tu nyumbani kwake pa kudumu, bali pia aliendelea kufundisha kwa miaka ishirini liyofuatia mpaka alipostaafu mwaka 1980.
Michango kwa Jamii
NNK alikuwa mtu wa tabia imara na uwadilifu aliyesimamia alivyovisadiki. Alisimama na mume wake hata kufikia hatua ya kupoteza kazi yake kwa muda. Alipigania na kusukuma mbele elimu kwa ajili ya wasichana na wanawake. Maeneo yake ya utaalamu yalikuwa ni pamoja na elimusiha, maarifa ya nyumbani, malezi ya watoto, ujengaji wa tabia na elimu ya kisomi kwa ujumla katika mpangilio wa chumba cha darasa. Alishiriki sana katika mambo ya Kanisa na alihudumu katika nafasi mbali mbali kama shemasi, Mkurugenzi wa Watoto na Shule ya Sabato na huduma za jamii nje ya Kanisa. Alikuwa si tu mpishi mzuri, bali mkarimu sana kwa watu wote kutoka Kanisani na Serikalini. Alikuwa kiongozi wa maburudisho kwa ajili ya Kanisa na viongozi wa kisiasa ikiwa ni pamoja na mawaziri. Mji wake ulikuwa kama hosteli kwa wageni wa Kanisa na wa familia. Amekuwa mchangamfu wakati wote na mwenye akili ya kutambua haraka hadi leo. Familia inayo furaha na heshima ya kumwita mama wa malkia.
Zaidi ya hapo, ujasiri na ustahimilivu aliouonyesha mama huyu katika maisha yake utasimama daima kama nguzo. Baada ya kutengwa kutoka kwa mume wake, alijitahidi kufundisha, kushauri na kuwaongoza katika makuzi watoto wake nane karibia peke yake. Hekima yake, mvuto na dhamiri vilizidi kwa mbali vya wanaume na wanawake wengi. Matokeo yake, watatu kati ya watoto wake walikuwa walimu wa mafanikio makubwa; mmoja akawa Mkurugenzi wa Huduma za Mapato ya Serikali huko Marekani, akisimamia uhasibu, huduma za mishahara na bajeti; mhandisi mmoja; nesi mmoja na wengine wawili wanaobakia wajasiria mali waliofanikiwa. Alifundisha wanawake pia maarifa ya nyumbani na ustawi wa jamii, akitoa semina za manufaa kwa jamii kila alipoishi. Hii ilikuwa hivyo hasa katika mikoa ya Mara, Mbeya na Kilimanjaro. Akiwa na umri wa miaka 97, bado yuko imara na akitoa majadiliano yenye faida na ushauri kwa wale wanaomtembelea. Kwa hakika anastahili kutambulika kama Sulemani wa leo.
Uzoefu wa Kimarekani wa NNK
Moja ya sifa kubwa ya kustajabisha ya Bibi ni nafsi yake ya mvuto mkubwa. Ana kipawa cha kuvutia watu wa aina mbali mbali bila kujali aendako. Maisha yake yamejaa visa vya jinsi alivyosafiri na kujipatia marafiki kila alipokwenda. Haikuwa tofauti Marekani. Mara tu alipowasili, alijipatia marafiki. Alihitajika kwa ajili ya kutoa visa vya umishonari katika makanisa mbali mbali. Mara mbili alialikwa mashuleni ambapo alielezea historia fupi ya Tanzania, kuanzia utumwa na kupitia utawala wa kikoloni hadi uhuru.
Mojawapo ya mambo anayojutia sana, ilikuwa kwamba hakujifunza kuongea Kiingereza bila shida. Na kwa hiyo, wakati akiwa Marekani, alichukuwa kozi ya Kiingereza kama lugha ya pili.
Mojawapo ya vipawa vikubwa vya Bibi kilikuwa kile cha upishi. Mara zote alikuwa na furaha alipokuwa anapika kwa ajili ya marafiki zake na familia. Mojawapo ya utaalamu wake ulikuwa mandazi yake maarufu yaliyojulikana kama “Mandazi ya Bibi.” Kupendwa kwa vyakula vitamu hivi na vya kufurahisha kulikuwa maarufu Tanzania na vile vile Marekani. Watu waliweza kusafiri kwa umbali na mapana ili mradi kupata sampuli ya “Mandazi ya Bibi.” Huko Marekani, vitamu hivi vya kuburudisha vilijulikana kama “mandolins,” “little pancakes,” “pancake cookies,” “funny doughnuts,” na “Bibi’s special cookies.”
Miaka ya Mwisho Final years
Bibi alikuwa na historia ya shinikizo la damu, ugonjwa wa mishipa ya moyo na moyo kushindwa kufanya kazi. Wakati akitembelea Tanzania kuanzia Desemba 2013 hadi Machi 2014, Bibi aliugua sana. Watu wengi walidhani kwamba ndio ulikuwa mwisho wa maisha yake, lakini Mungu alinusuru maisha yake na aliweza kurudi Marekani. Alikuwa amedhoofika, lakini alikuwa anaweza kutembea kwa msaada wa kifaa maalum…hasa ndani ya nyumba. Usiku wa Jumapili ya tarehe 7 Septemba 2014, alikuwa mzima wa kutosha kubariki chakula na alisali vizuri sana. Wakati huo alikuwa macho na akifuatilia mambo vizuri. Baadae alielekea kitandani, akisaidiwa na mjukuu wake, Nampombe ambapo moyo wake ulishindwa kufanya kazi na akaanguka. Familia yake ilimfanyia CPR wakati wakisubiri waganga wasaidizi kufika. Waganga wasaidizi walijitahidi kumrudishia fahamu na baada ya muda waliweza kupata mapigo ya moyo. Baada ya hapo, Bibi alisafirishwa kwa kutumia gari la wagonjwa na kupelekwa hospitali ya UCLA. Wakati familia yake ilipowasili, walipewa taarifa kuwa madaktari wamefanya kila kitu walichoweza kufanya lakini inaonekana mwili wake ulikuwa umechoka na moyo wake ulisimama tu kudunda.
Kumbukumbu yake itahifadhiwa kwa upendo mkubwa na: watoto watatu wa kiume, Ferdinand (Sala), Aggrey Chambi (Witness), na Peter (Antonieta); watoto watatu wa kike, Snow, Pheno, na Margaret (Sam); wajukuu 37, vitukuu 21na vilembwe 12 pamoja na kundi kubwa la watoto wa kaka na dada zake na mabinamu. Atakumbukwa pia na familia zake za Kanisani, wafanyakazi wenzake wa zamani na wanafunzi, na marafiki wengi na ndugu.